Tuesday, May 29, 2007

Viongozi wa dini na vikombe vya farao

Na Nyasigo Kornel

Askofu wa Kanisa la Anglikani katika Jimbo la Johannesburg Desmund Tutu katika hotuba yake mwaka jana kwa viongozi wa dini wa Kanisa hilo anasema kuwa sasa hivi matendo ya huruma kwa jamii inayoteseka na kuonewa uonyeshwa zaidi na asasi zisizo za kiserikali ‘NGOs’ kuliko madhehebu ya dini ambayo ingetegemewa kuwa hii iwe moja ya majukumu yake.

Desmund anatumia lugha ya picha akisema kuwa viongozi wa dini wasiwe watu wa kujiandae kusoma ibada za mazishi kwa vifo ambavyo wangeweza kuzuia.

Kunapotokea udhalilishaji wa haki za binadamu kama suala la wafungwa kutotendewa kama binadamu ambalo sasa hivi ni mada kubwa sana Tanzania, utasikia asasi kama vile Legal for Human Right Centre (LHRC) mkurugenzi wake akiongelea na kutetea haki za watu kama hawa.

Hii inashabihiana na malalamiko ya Negul Showman katika kitabu chake kiitwacho ‘Strong only on our eyes’ akisema kuwa viongozi wa madhehebu ya dini kila mara wanapokutana na viongozi wa serikali wamejikita sana katika uchangishaji wa pesa kwa ajili ya ujenzi wa makanisa na misikiti ‘fund raising’.

Wafungwa wetu wanapata adhabu ya aina nyingi sana, zingine ni za kisaikolojia na zingine ni za kimaumbile ikiwemo ya kuwa mbali na familia zao, kutokuwa na uhuru, kula mara moja kwa siku na kufanyishwa kazi.

Adhabu kama hizi zinatosha, sio vema tena kama ilivyo sasa wanalala kwenye chini kwenye sakafu bila magodoro, hawana mashuka, wanakujisaidia kwenye ndoo inayowekwa ndani ya sehemu yao ya kulala na wakati mwingine wanapigwa.

Mazingira kama haya yamefikia hatua wafungwa wengine kufa au kuugua kwa kiasi kibaya.

Mtu anapofika jela kwa siku ya kwanza upekuliwa akiwa uchi wa mnyama, askari uangalia hadi katika sehemu zake za haja kubwa kama ameficha bangi au kitu ksichotakiwa.

Ukifika katika hospitali utakuta mfungwa ameugua yuko hoi lakini ana pingu mguuni na mkononi, unashindwa kujua kama huyu naye bado ni binadamu au ameachwa katika kundi lile la watu tunaowaita ‘hata akifa hana faida yoyote’.

Mtetezi mmoja wa haki za wafungwa ambaye ni mzungu wa huko Ulaya Dustan Panther ndiye amewahi kujitokeza katika majukwaa ya Afrika na kukemea jinsi tunavyowatendea wafungwa wetu huku sisi wenyewe tukihubiri usawa wa binadamu.

Jimmy Larry aliwahi kuandika makala yake katika gazeti la ‘The Private Eyes’ la tarehe 12 Julai 2001 akitoa maoni kuwa ni vema wafungwa wawe na kikundi chenye nguvu cha kuwasemea ili hali zao ziboreshwe.

Haitoshi tu kwa ahadi alizotoa Rais Jakaya Kikwete, yeye anaweza akawa na nia ya kuwaboreshea wafungwa hali zao za maisha, lakini mabadiliko haya yalisemwa kisiasa sana na hadi sasa jela zetu hazijabadili namna wanavyowatendea wafungwa wetu.

Lazima kuwepo na kikundi chenye nguvu na chenye kuleta msukumo.

Katika Biblia, mfano wa Musa ni mfano wa wachungaji na mapadri kuiga, alipokuwa akiwaongoza wana wa Israeli kuwatoa utumwani Misri alishirikina na waisraeli katika kila adha iliyowakumba. Mwingine ni mfalme Daudi, yeye aliweza hata kupigana na adui zake kutetea kundi lake, hata mfalme Solomoni.

Sasa viongozi wetu wa dini watuambie wao ni wa mfano wa nani?

Mtaalamu wa elimu ya dini ‘Theolojia’ Prof. Leonardo Boff anaandika katika kitabu chake ‘Church: Charism and Power’ akisema kuwa kosa kubwa wanayofanya watumishi wa Mungu ni kuwa na dhana potofu kuwa sakramenti wanazowapa watu zinauwezo wa kufanya kazi peke yake.

Kwa miaka mingi makanisa yamekuwa yakiandaa watu kuwa wanyonge na hivyo serikali mbalimbali duniani imekuwa ikitumia dini kama chombo cha kuwaandaa watu kuwa watiifu kwa lolote na hatima yake ni kuwa imekuwa mhimili wa kukomaza unyonge wa kifikra na maamuzi.

Katika karne ya 13, 14 na 15 kanisa Katoliki ilijawa na dhana ya ubinafsi kuwa ni yenyewe pekee ndio ilikuwa na ukweli wa kiimani na maisha na wale wote ambao hawakuamini juu ya Ukatoliki waliuawa.

Na kwa jinsi hii maelfu ya watu waliuawa kama waalifu wa kiimani.

Leo hii kanisa hilohilo limegundua kuwa lilikuwa linakeuka haki za kimsingi za binadamu, uhuru wa kifikra, uhuru wa kuabudu na kuamini.

Hata hivyo wachambuzi wa kisiasa wamekuwa wakilishangaa kanisa hilohilo lililokuwa na nguvu nyingi sana kisiasa kipindi cha biashara ya utumwa kwa kunyamaza kimya wakati Waafrika wakiuzwa kama wanyama katika biashara hiyo.

Kanisa hilo hilo lilinyamaza kimya wakati Wahindi Wekundu wa Amerika wakiteketezwa.

Na kwa sababu hii Papa John Paulo II aliomba msamaha wakati wa maandalizi ya jubilee ya mwaka 2000.

Kwa muda wa miaka 5 tu Papa John Paulo aliomba msamaha mara 94 juu ya makosa haya.

Kadhalika makanisa yawe ya Kiislamu, Kilokole, Kiprotestanti na Katoliki wanakosea sana kunyamaza kimya wakati makosa kama haya ya wafungwa na watuhumiwa ambao ni mahabusu kuishi kama wanyama, wakati ni watu walio na haki ya kuishi wakiwa na afya nzuri baada ya kutumikia kifungo chao.

Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kuwaambia viongozi wa dini katika hotuba yake aliyoitoa nchini Marekani kwa wamisionari wa Marynol Fathers akisema kuwa unapoona matatizo ya kimaadili yameongezeka katika jamii basi ujue kuwa kanisa limeshindwa kuwajibika.

Vinginevyo huko mbeleni wasipojirekebisha na kupenyeza dhana kuwa dini ni kwa ajili ya maisha ya hapa duniani na mbinguni basi madhehebu ya dini na ibada zao zitaonekana kama sehemu za biashara na vikundi vya kijamii ambayo mtu huweza kuitumia kwa maslahi binafsi na kujiongezea sifa za kijamii.

Haitoshi tu mhubiri kutembea na daftari kuandika orodha ya wafungwa waliokoka, huku akijivunia idadi ya hao wafungwa nali akisema kuwa Mungu amempa upako wa kutumikia wafungwa.

Mwandishi mmoja wa anayeandika vitabu vyenye uatat sana Marekani Hugh Hewitt katika kitabu chake cha ‘The Embarrassed Believer’ anaandika kuwa imetosha kuwahubiria wanyonge unyonge na kuwapoozesha kumaliza maisha ya duniani kwa machungu yanayoweza kukwepeka.

Mwandishi huyo anaona makosa makubwa sana ndani ya viongozi wa makanisa na nasema kuwa imefikia hatua Mapadri, Mashehe, Wachungaji na Wainjilisti kuanza kuangalia upya mapambano yao, inawezekana wakijaza chuki kati ya muumini na shetani huku akimkemea shetani kila siku kumbe kama wangesaidia kupiga kelele ili kufanyike mabadiliko.

Kama viongozi hawatabadilisha ukimya wao na kuwa Askofu wa kanisa la Anglikani ya Johannesburg Desmond Tutu aliyepata tuzo la Nobel mwaka 1984 kwa kutambua kuwa Mungu haonekani katika maisha ya watu kama watu hawana cha kuvaa, wanaonewa, hawana amani, hakuna utawala wa sheria na mengineyo.

Lakini sisi tumegeuza makanisa na sehemu za ibada kama sehemu za kukujikusanyia.

Yesu angewaogopa Mafarisayo na kuwakemea ili apate sifa basi angefanana na hao Mafarisayo.

Viongozi wa dini msijifiche makanisani na kusahau dhiki wanazopata wahumini wenu la sivyo ibada zenu hazitakuwa na maana katika uhalisia wa maisha.

No comments: