Tuesday, May 29, 2007

Mwathirika wa Operesheni ilimng’atusha Mwinyi apatikana jalalani


Na Nyasigo Kornel

Mzee Nhalilo Ikerenga Mkigila (65), mmoja wa walioteswa katika ‘operesheni ya wachawi’ mkoani Shinyanga ya mwaka 1974 iliyomfanya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ajiuzulu Uwaziri wa Mambo ya Ndani, anaishi kama mbwa koko jijini Dar es salaam.

Akizungumza na Mtanzania jana Nhalilo ambaye amelemaa mkono na makovu mengi mwilini kutokana na mateso akiwa gerezani, alisema kuwa amekuwa akipata riziki kwa kuokota na kula makombo kwa mama-lishe wa Posta Baharini na kulala stesheni ya reli Posta.

“Watu wengi wanafikiri kuwa mimi ni kichaa, la hasha, mimi nina familia yangu na inaishi Sengerema katika kijiji cha Nyamabano-Nyanzenga, huku nimekuja kutafuta haki zangu na nilipokoswa nauli ya kurudi nyumbani niliona sehemu salama ya kulala ni stesheni kwa maana ni karibu na kituo cha polisi,” alisema Nhalilo.

Alisema kuwa mwaka 1974 Serikali ilieendesha operesheni ya kukamata watu waliotuhumiwa kuwa ni wachawi na ndipo alikumbwa na huo mkasa kijijini kwake Manonga Wilayani Maswa hata kuwekwa mahabusu katika gereza la Nhumbu- Shinyanga sehemu anasema kuwa alikuwa akipata mateso ya kinyama hata kumsababishia athari za kaiafya na hata watu wengine 6 walikamatwa katika mkumbo huo kufa baada ya muda mfupi.

“Tulikuwa tunachapwa kwa viboko, tunapakwa maji ya pilipili kwenye njia ya haja kubwa, kwenye sehemu zilizochubuka baada ya kuchapwa, wanawake walikuwa wakipakwa kwenye sehemu zao za siri, machoni na hata kuna kipindi ilinisababishia upofu,” alisema.

Alisema kuwa wanaume na wanawake katika gereza hilo walikuwa wanavuliwa uchi na kuwekwa sehemu moja huku mateso haya ya kinyama yakiendelea, anasimulia jinsi ambavyo walipokuwa wanaamishwa katika gereza la Mwanholo mkuu wa gereza la kwanza aliwasomea dua akisema.

“Ndugu zangu kutoka Shinyanga naomba Mungu awasaidie mrudi salama, mtakwenda Mwanholo mtakayoyaona huko naomba Mungu awasaidie mrudi salama,” alisema mkuu wa gereza la Nhumbu.

Nhalilo alisema anaidai serikali fidia kwa sababu mahakama ilithibitisha kuwa hawakuwa na hatia na kuachiliwa huru huku yeye akiwa ameathirika kiafya ikiwemo kulemaa mkono na macho yalipopofuka na vilevile alipoteza vifaa vyake vya uganga.

“Mimi nilikuwa ni mganga wa kienyeji na wala sikuwa mchawi, walininyang’anya vifaa vyangu vya uganga na hivyo lazima wanilipe fidia,” alisema.

Ingawaje huyu mzee hana elimu kubwa na kuishi mazingira magumu sana, aliweza kutunza nyaraka zake zote kwenye mkoba wa ngozi aliyokuwa akitembea nayo kila alipokuwa akienda.

Operesheni hii iliendeshwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa (Area Commissioner) kwa kipindi hichi Michael Mabawa ambaye alikuwa akituma polisi kukamata watu waliohisiwa na jamii kuwa ni wachawi.

Michael Mabawa baadaye alistaafishwa kwa manufaa ya umma kama vile Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi alivyostaafu Uwaziri wa Mambo ya Ndani kwa tuhuma ya vitendo hivi vya kinyama kufanyika katika Wizara yake.

Ingawaje hawa walistaafu lakini Mwinyi alikuja baadaye akawa Rais wan chi hii na Michael Mabawa alikuja kugombea tena Ubunge katika jimbo la Magu na kushinda kwa kipindi kimoja kabla ya kuaga dunia.

Nhalilo aliwahi kwenda kupeleka madai yake kwa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) walimpooza tu na kumwambia kuwa arudi kwake Sengerema mpaka watakapomwita, ahadi ambayo haijafanyika mpaka leo.

Kutokana na maelezo yake mzee huyu aliwahi kutoa malalamiko yake mbele ya Hayati Mwl. Julius Nyerere ambapo alipewa nauli za kumrudisha kwake na kisha Mwalimu Nyerere alimwandikia barua ambayo Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Maswa wakati huo akiitwa ‘DD’ alikataa kumpatia, suala linazusha imani yake kuwa Mwalimu Nyerere alimwandikia kujibu madai yake.

Mzee huyu ambaye ndugu zake walikuwa wameshafanya msiba wake mwaka 2005 wakiwa na imani kuwa ameshafariki, habari zake zimepatikana siku chache tu baada ya mtu aliyemtambua kumhoji.

No comments: