Tuesday, May 29, 2007

Mtaalam aonya kuhusu madini ya Uranium


Na Nyasigo Kornel

Watu wanaokaa katika maeneo yaliyogundulika kuwa na madini aina ya Uranium wako katika hatari ya kupata kansa ya mapafu inayosababishwa na hewa aina ya Radoni inayotolewa na madini hayo.

Mkuu wa Idara ya Jeolojia katika kitivo cha sayansi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dr. Isaac Marobhe alisema hayo jana ofisini kwake katika mahojiano maalum na gazeti hili.

Dr. Marobhe anasema kuwa kinachofuatia baada ya sigara kwa kusababisha kansa ya mapafu ni hewa hatari ya Radoni.

Anasema kuwa mtu akijenga nyumba juu ya mawe hata kama yako chini sana, hewa ya Radoni hupenya na kujaza nyumba hata mkaaji anapopumua uivuta hewa hii.

“Nchini Marekani tu watu 160,000 hufa kila mwaka kutokana na kansa ya mapafu kati ya hao watu 21,000 wanaokufa kwa kansa husababishwa na hewa hii hatari,” alisema Dr. Marobhe.

Hapa Tanzania madini aina ya Uranium imegundulika kuwepo sehemu nyingi ikiwepo Bonde la mto Rufiji, Songea, Bahi-Dodoma karibu na Manyoni, Milima ya Uluguru na Garula-Mbeya.

Kwa mujibu wa huyu mtaalamu, madini ya Uranium inatabia ya kuoza na hivyo inapooza inatoa chembechembe inayoitwa gamma, alfa na beta pamoja na hewa hii inayoitwa radoni iliyo na uwezo wa kupita katika ardhi na kujaa ndani ya nyumba iliyojengwa juu ya eneo ilipo madini hii hata kumwathiri mkaaji, na hasa kama nyumba haina mfumo mzuri wa kupitisha hewa.

Anasema kuwa chembechembe aina ya alfa na beta hazina madhara sana kwa sababu zinazuliwa kupita hata na jiwe lenye unene kiasi cha sentimita 30 tu na hivyo chembe iliyo na uwezo wa kupenya ni gamma tu.
Ripoti iliyoandikwa katika jarida la mambo ya tiba itwayo Pubmed inasema kuwa atomi moja tu ya radoni ina uwezo wa kusababisha kansa ya mapafu na hivyo zio lazima mpaka uwe nayo kwa wingi katika mapafu yako.

Jarida hilo linaandika kuwa hewa hii uua mfumo wa kuzaliana kwa seli za mapafu hivyo huziminya seli hizo na kasha kuziua na kumsababisha kansa ya mapafu.

Jarida hilo pia linatoa takwimu kuwa asilimia 30 ya vifo vya watu wa Iroshima na Nagasaki sehemu ilipoangushwa bomu la atomiki na Wamerakani katika vita vikuu vya pili vya dunia inasababishwa na kansa ya mapafu.

Dr. Marobhe anasema kuwa katika nchi zilizoendela katika kuzingatia afya ya jamii wanapima hata mawe ya kujengea nyumba kama ina kiasi cha mionzi ya radiesheni.

“Mawe aina ya ‘granite’ kwa kawaida ina kiasi Fulani ya mionzi ya radiesheni inayoweza ikasababisha kuwepo kwa hewa hii ya Radoni, hivyo ujenzi wa kutumia mawe ovyoovyo pia inaweza ikamweka mtu katika mazingira ya athari,” alisema Dr. Marobhe.

Anasema kuwa hata walipokuwa wanapima kwa kutumia ndege (Airbone geophysics) waligundua kuwa madini aina ya Phosphate iligunduliwa kule Arusha katika eneo la Minjingu ilikuwa na chembechembe za Uranium na hivyo lazima kuna hewa ya Radoni.

Alishauri kuwa serikali ifanye kila iwezalo kuwaamisha wakazi wa maeneo yaliyo na madini haya ili wasipatwe na madhara makubwa kama ya kansa ya mapafu.
Mwisho

No comments: