Tuesday, May 29, 2007

Neno ‘umaskini’ lilivyotumika kupumbaza Waafrika


Na Nyasigo Kornel

Ripoti ya mwaka huu wa utafiti wa kampuni ya Marekani ijulikanayo kama Federated Media Inc inasema kuwa katika kila hotuba ya viongozi wakuu wa mataifa makubwa -G8 kwa nchi za Kiafrika lazima ionyeshe na kusisitiza kuwa bara la Afrika ni maskini.

Neno umaskini limetumiwa sana kama propaganda dhidi ya bara ya Afrika na nchi za magharibi kiasi kwamba imefikia hatua imeingia katika akili zetu na viongozi wetu wa Waafrika wameimanishwa kulihalalisha hilo neno kujifichia kama kichaka pale wanaposhindwa kutimiza malengo yao kwa jamii.

Mnaijeria John Oguefi mwandishi wa kitabu kiitwacho ‘The Brain Cancer Syndrome’ anasema kuwa ‘Umaskini’imeshaingia katika akili ya vizazi vyetu na kuweka ugonjwa mkubwa sana utakaotuchukua miaka mingi sana kuondoa.

Gazeti la The Washington post la 23 Januari 1981 ilichapa sehemu ya ripoti mtaalam mmoja wa saikolojia ya propaganda za kisiasa (Political propaganda psychology) Dr.Denis Amando aliyewahi kuandika ripoti yake kwa shirika la Kipelelezi la nchini Marekani -CIA akishauri kuwa CIA ikitaka kuharibu na kudumaza jamii yoyote ya watu mbinu moja kubwa ni kuwapa taarifa mbovu yenye kuwaonyesha kuwa jamii ile ni dhaifu.

Si mara moja utasikia viongozi wa nchi wakihutubia wananchi hata pale wanapokuwa wanazindua mradi mkubwa na mzuri wenye mafanikia utawasikia wakisema, “Pamoja na umaskini wetu lakini tumejikokota… ingawa Tanzania ni maskini… sisi ni nchi maskini duniani”.

Tume nyingi duniani zimeanzishwa na nchi za Magharibi na hasa Rais wa Marekani George Bush na Waziri Mkuu wa Uingereza Tonny Blair na zote zinaingiza dhana ya umaskini kwenye vichwa na nyoyo za Waafrika.

Aliyekuwa Rais wa Marekani Bill Clinton anataka kupunguza umaskini Afrika kwa mpango anaouita ‘Poverty Reduction Strategies’, Rais wa sasa wa Marekani Bush naye eti anataka kuondoa umaskini Afrika kwa kutumia ‘Millennia Challenge Account-MCC’ na rafiki yake Blaie anataka kuondoa Afrika katika umaskini Afrika naye anakuja na wazo lake linaloitwa ‘Poverty Elimination scheme’.

Gazeti la The Times la London Uingereza la mwezi Octoba 21, 2004 ukurasa wa 6 lilitoa kejeli likitoa takwimu kuwa asilimia 95 ya safari za viongozi wa bara la Afrika huko Ulaya na Marekani ni za kuomba misaada ya kipesa.

Lilipofikia hatua UKIMWI ulikipoonekana umeenea sana katika kusini mwa Jangwa la Sahara na hasa Afrika kwa ujumla Ulaya na Marekani kwa kutumia vyombo vyao vya habari zikaeneza propaganda kuwa UKIMWI ni ugonjwa wa watu maskini.

Hata Rais wa Afrika ya Kusini alishawishika kutangaza katika vyombo vya habari kuwa UKIWMI ni ugonjwa wa nchi maskini huku asasi mbalimbali na wasomi wakimnukuu kwenye tafiti zao.

Walisahau kuangalia nchi tajiri sana katika Afrika kama Botswana lakini bado inaoongoza kwa maambukizo ya UKIMWI huku ikiwa na asilimia 36 ya watu wake wameathirika huku miji kama New York alikaririwa Meya wa mji huo akilaumu serikali ya Marekani kutoa pesa nyingi nje ya mipaka yake kupunguza maambukizo ya UKIMWI na kusahau mji huo ambao unaingiwa na wageni wengi kila leo huku ikiripotiwa kuwa waathirika wengi sana wa UKIMWI lakini serikali yao hairuhusu kutoa takwimu sahihi.

Imefikia hata katika silabasi na mitaala yetu ya masoma ya taaluma ya maendeleo (Development studies -DS) kwa chuo kikuu karibia kila mada ina uhusiano na ‘umaskini’ na kama hujui sawasawa mada ya umaskini (poverty) uwezekano wa kumshawishi muhadhiri wa chuo kikuu wa masomo ya DS ni kazi sana.

Umaskini imepandikizwa sana katika akili yetu na ni wakati wa kubadilika kuwapa watu mwamko mpya na kuwapa watu nafsi yenye kujiamini.

Ukifika maeneo mengi katika jiji la Dar es salaam utakuta mtu anaona mtaro wake umejaa maji taka lakini haioni kama ni tatizo, hajitumi kuondoa takataka zilizoziba mitaro mpaka asubiri serikali ya mitaa ikaite magari yale ya BUDEKO.

Mbwa akifa mtaani watu wako radhi waumie kwa harufu mpaka pale maghari ya Halmashauri ya mji yatakapokuja kuzoa takataka pale.

Umaskini wetu utaona kuwa umebebwa akilini sana kuliko katika miundo mbinu zilizopo.

Wataalamu wa elimu ya teolojia na hasa katika nyanja ya umisionari kama Leonardo Boff anaamini kuwa ukimwathiri mtu katika akili mara moja umeathiri na roho yake na ndio maana unaona madhehebu mengi sana yamefanikiwa mujenga mahekalu makubwa kwa kukusanya pesa za watu maskini.

Hivyo kama tutafanikiwa kujenga upya fikra za watu wetu juu ya mtazamo wa umaskini kama changamoto na sio kama kushindwa basi Tanzania itaomba misaada michache sana kutoka Ulaya na Marekani.

Historia inaoonyesha wazi kuwa Afrika inaendelea na kukua kwa kasi kuliko bara lolote lile lilowahi kuwepo duniani pamoja na kuwepo na pingamizi nyingi kwa mataifa makubwa na mashirika yao ya kuinyanyasa Afrika kama Shirika la Biashara la Dunia -World Trade Organization na Shirika lapesa la Kimataifa - IMF.

Maendeleo yaliyoichukua Ulaya miaka 400 kuyafikia Afrika imeifikia kwa nusu ya karne, lakini haya yote hawayakubali na hawataki CNN, BBC, DW na vyombo vyao kuionyesha Afrika kuwa ina uhai wa kimaendeleo.

Umaskini wetu umezidishwa na vyombo vya habari za Ulaya na fikra zetu zimehalalisha haya kwa kusisitizwa na viongozi wetu kuwa sisi ni maskini na imani yetu itaendelea katika kuamini umaskini kwani hata wassomi wetu wakubwa wanakumbatia imani hii.

Mwaka jana Jaffery Sach msahauri wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan aliwahi kutoa ripoti kwa vyombo vya habari akisema kuwa karibia asilimia 60 za tafiti zote zinazofanywa katika nchi maskini duniani zinahusu umaskini.

Aliendelea kusisitiza akisema kuwa wakati Ulaya na Marekani zikifanya utafiti juu ya teknolojia na mbinu kandamizi za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni, wasomi wa Afrika haipati fursa za kuzijua mbinu zao kwani wengi wameinamisha vichwa vyao kwenye kutafiti juu ya umaskini na kuusisitiza kwa wananchi wao.

Umaskini upo Afrika ila umezidishwa mno na nchi za Ulaya na Marekani kwa kuwatumia viongozi wetu na wanasiasa wetu wanaopokea vitu bila upembuzi yakinifu.

Wanatueleza hali ya umaskini wetu kwa kiwango ambacho hata kinatushangaza sisi tunaoishi hapa katika huo umaskini.

Viongozi, wasomi, asasi, viongozi wa madhehebu ya dini, mitaala yetu na vyombo vya habari vianze kuwajengea watu hali ya kuondokana na fikra za kimaskini.

Biblia husema kuwa chochote unachokishuhudia kwa kinywa chako ndicho kinachokutokea.

0715 551455
emmakornel@yahoo.com


No comments: