Tuesday, May 29, 2007

Falsafa ya maandishi ya khanga kwa fikra za mwanamke

Na Nyasigo Kornel

Mwanasaikolojia wa mambo ya ushauri kwa watu walio na fadhaa na mashaka katika maisha (psychotherapist) Dr. John Robert katika kitabu chake kiitwacho ‘The sense of women’, kitabu kilicholaaniwa sana na wanaharakati kuwa kimemwonyesha mwanamke kama kiumbe kinachotumia hisia zaidi kutoa uamuzi kuliko akili.

Dr Robert anasema katika ukurasa wa 12 wa kitabu hicho kuwa mwanamke anaweza akapata tiba ya fadhaa, mashaka, wasiwasi na maudhi yake hata kwa kusoma maandishi chanya (yaani maandishi yanayounga mkono matakwa yake) hata kama inamdanganya na hilo suala haliwezekani.

Hivyo mwanamke aliyekosana na jirani yake mwanamke huweza kujisikia furaha kuvaa khanga yenye maandihi yanayomtetea yeye na kumsimanga jirani yake aliyetofautiana naye hata kama ule ujumbe hauna hauna ukweli.

Mtaalam wa Saikolojia Huston Marawasa aliwahi kuandika katika jarida iitwayo ‘The Riddles’ akiamini kuwa hisia, iwe hasira au furaha zinaweza kurekebishwa na kuwa kwa kiasi cha wastani hata kwa kujilisha kwa taarifa za uongo, ili mradi tu zile taarifa ziwe zimemfikia mhusika kwa namna ya kuiamini.

Na ndio maana katika mashairi ya William Shakespeare aliwahi kuandika huku akijibizana na Othello huku Shakespeare akisema kuwa ‘there is no true love without lies’ (hakuna mapenzi ya kweli bila kuwepo na udanganyifu) na mwishoni mwa shairi hilo anamwambia Othello kuwa ‘when my lover tells me lies, I know that I am cheated but I simply believe’ (ninapoelezwa suala la uongo na mpenzi wangu ninakuwa ninajua kuwa ninadanganywa lakini najikuta naamini).

Haya mawazo ya Shakespeare na Huston yanatoa picha halisi kuwa mtu anaweza akapumbaza fikra zake ili ajijengee imani itakayompa usalama zaidi katika roho kuliko kuwa na mashaka isiyokuwa na majibu yanayoweza kuleta utatuzi wa haraka.

Mzee Felix Hassan Ndonjo ana miaka 67 sasa na aliwahi kuwa mtaalamu wa mavazi, ubunifu na urembo, amewahi kufanya kazi katika kiwanda cha nguo cha Musoma Textile Limited (MUTEX) katika upande wa maandishi ya mavazi.

Ndonjo anasema kuwa yeye alikuwa akiangalia migogoro aliyonayo mwanamke katika msiaha yake ya kila siku na kisha uyatatua kwa njia ya maandishi ya khaga.

“Migogoro ya kifamilia au kati ya familia moja na nyingine ni suala la kawaida lakini utajikuta kwamba wanawake walio wengi ndio waathirika wa majanga ya kijamii, hivyo chuki nyingi za familia huwa katika roho ya mwanamke,” anasema Ndojo.

Ndonjo nasisitiza kuwa maandishi ya khanga ni tiba kwa wanawake wengi na hasa wanawake wa kawaida (anaimanisha mwanamke mwenye elimu ya kiasi na uchumi wa kubangaiza).

Rafiki yake mzee Ndonjo waliyekuwa naye katika idara moja mzee Ogutu Dera mkazi wa Musoma vijijini kwa sasa anasema kuwa yeye alikuwa na uwezo wa kwenda katika mitaa ya uswahilini na kusikiliza masimango ya akina mama na kisha anapata mawazo juu ya falsafa ya kuandika maandishi ya khanga.

Anasema kuwa siku moja alikuwa akilala chumbani kwake katika mtaa wa Iringo karibu kabisa na Bandari ya Musoma, akiwa katika nyumba ile iliyokuwa na wapangaji wengi alisikia mwanamke mmoja akimsengenya mke wake akisema, ‘Maskini akipata matako ulia mbwata’.
“Nilichukua msemo huu wa kawaida na kisha baada ya wiki mbili nilipewa khanga kutoka katika duka la ushirika na niliwauzia kwa mkopo, yule mwanamke alinunua ile ile khanga na kisha kulianika kila siku kwenye kamba mbele ya nyumba yetu ili mradi tu amuumize mke wangu,” anasema mzee Dera.

Khanga ni vazi linalovaliwa na wakazi wengi wa Afrika ya Mashariki ikiwa imeletwa katika karne ya 19 na wafanyabiashara wa Kiindi na Waarabu.

Mwanzoni ilichukuliwa kama bidhaa kwa wakazi wa Pwani tu na hasa hasa Zanzibar, lakini baadaye imekubalika kwa Tanzania yote na sehemu kubwa ya Afrika ya Mashariki na kati.

Khanga inavaliwa sana na wanawake na baadhi ya wanaume ushona mavazi yao kwa kutumia vitenge.

Katika khanga utakuta maandishi yenye misemo, mafumbo na methali mablimbali ambayo mara nyingi umfanya mwanamke kuchagua khanga ya aina Fulani na kuacha nyingine.

Kwa mfano katika khanga utakuta maandishi kama vile ‘Ajabu nazi kavu kutaka kuvunja jiwe’, hapa mwanamke anajivika uhusika wa jiwe na mwenzake anamvika uhusika wa nazi huku yeye akiishawishi fikara zake kuwa anao uimara kama wa jiwe katika hilo suala wanaloling’ang’ania na mwenzake ni dhaifa mbele ya jiwe kama nazi.

Hivyo atakapopita mbele ya mwanamke mwenzake au hasimu wake anajisikia katika roho yake kuwa amekuwa mwamba mbele kwelikweli.

Katika kitabu cha ‘The heart of woman’ mwandishi Handy Casgert anasema kuwa mwanamke ana nguvu nyingi za kijamii moyoni na hivyo masuala ya kijamii na mahusiano yanampa shida nyingi sana kuliko mwanaume na akasema kuwa ujumbe mfupi wa simu za mkononi, ujumbe chanya katika barua, ujumbe chanya wa mziki zina manufaa na tiba kubwa kwa roho ya mwanamke kuliko ya wanaume walio wengi.

Mwisho


No comments: