Showing posts with label Jamii. Show all posts
Showing posts with label Jamii. Show all posts

Tuesday, May 29, 2007

Makumbusho ya Mwalimu Nyerere: Kutoka Nyumba ya Udongo hadi Ikulu

Na Nyasigo Kornel

Huwezi ukasubiri kuambiwa, kwa mara ya kwanza ukifika Mwintongo- Butiama maali alipozaliwa baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere utaona kila hali ya maisha ya mtu wa kawaida na sio kama viongozi wengi wanaojijengea mahekalu na kuweka vizuio katika nyumba zao.

Inawezekana hii pia ikawa imechangia hata kanisa Katoliki kumwona na kumtangaza mwenye heri.

Makumbusho ya Mwalimu N yerere ipo Butiama katika Mkoa wa Mara upande wa kaskazini mwa Tanzania.

Makumbusho haya yalizinduliwa tarehe 2 Julai 1999 na aliyekuwa Waziri Mkuu mheshimiwa Frederick Sumaye.

Butiama ni maali alipozaliwa na ndipo alipozikwa baba wa Taifa Mwalimu J.K Nyerere.

Makumbusho yalianzishwa ili kukusanya, kutunza na kuonyesha vitu vyote ya kitaifa na kimataifa vilivyohusu maisha ya mwalimu J.K Nyerere.

Mwalimu alifariki dunia 14 Octoba 1999 na kuzikwa huko Butiama.

Ukifika Butiama, kuna mambo machache sana yanayoweza kukuthibitishia kuwa kijiji hiki ndicho kilichomzaa na kumlea mwana wa Afrika.

Kutoka katika nyumba iliyojengwa kwa udongo ndipo alipolelewa mtoto aliyeikomboa Tanzania na Afrika katika makucha ya mabepari na mabeberu.

Hakuna uzio kuzunguka kwake, wanawake na watoto huchota maji nje ya huo mji na hata kufua nguo kitu ambacho watu wengi katika ngazi ya Mwalimu wasingekubali.

Barrick North Mara: Chachu ya maendeleo Tarime


Na Nyasigo Kornel

KABLA ya kuitwa Barrick North Mara ilikuwa ikiitwa East African Gold Mine iliyoanzishwa mwaka 1993 na kupata leseni na kuendesha shughuli za uzalishaji mwaka 1996.

Barrick North Mara waliweka mtambo wao wa kwanza wa uzalishaji 2002 na hapo ndipo mara moja mgozi uliona umuhimu wa kusaidiana na wakazi wa Nyamongo kuboresha maisha yao.

Ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka mgodi wa dhahabu ya Barrick North Mara iliyopo Nyamongo katika Wilaya ya Tarime wananufaika na uchimbaji huo unaoendelea katika eneo hilo, Barrick North Mara imekuwa na shughuli mbalimbali za kuikwamua jamii katika hali ngumu ya kimaisha.

Mgodi wa Barrick imewajenga nyumba za kisasa zipatazo 96 kwa wale waliohamishwa kutoka katika maeneo ambayo uchimbaji unapofanyika. Nyumba hizi ni za kisasa kabisa zinazoweza kukimu familia kubwa.

Baadhi ya wananchi wanaozunguka mgodi huu walipewa zabuni za kujenga nyumba za kisasa kwa ajili ya wanavijiji wanaohamishwa ili kupisha shughuli za migodi.

Hii ilifanyika ili kuwaongezea ajira wakazi wanaozunguka mgodi huo wa North Mara.

Hata hivyo mgodi uliona kuwa sio vema mtu kukaa katika nyumba ya kifahari huku umaskini ukiwa bado unamzingira, na ndipo ulipoanzishwa chama cha kuweka na kukopa cha Mara SACCOS iliyo na wanachama zaidi ya 500 toka kuanzishwa mwaka jana.

SACCOS hii ilipoanzishwa kampuni iliwagharamia baadhi ya wanachama ziara za kwenda kujifunza katika benki zinazofanya kazi chini ya mtandao wa vyama vya kuweka na kukopa nchini maarufu kama Dunduliza Kanda ya Ziwa.

Lengo ilikuwa ni kwamab SACCOS iweze kutoa mikopo ya fedha yenye riba nafuu kwa wanachama wake ili kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza miradi ya uzalishaji mali ili kuwaongezea kipato na kupunguza umaskini miongoni mwao.

Kwa ajili ya kuondokana na umaskini wa kipato, mgodi vilevile ulianzisha mpango maalumu wa kuwakopesha wananchi ng’ombe wa kisasa wa maziwa, na kasha mwananchi alitakiwa kulipa ndama wa kwanza na wa tatu tu na kisha ng’ombe wake aliachiwa.

Hii imewaongezea kiwango cha uzalishaji wa maziwa kwa ufugaji uliogharimu malisha ya mbali na hivyo kuboresha utunzaji wa mazingira.

Maziwa yanayopatikana uuzwa Sirari, na mahusianao kati ya Nyamongo na Sirari ni muhimu sana na hivyo mgodi uliamua kujenga barabara kati ya Sirari na Nyamongo kilomita 56 kwa kiwango cha lami.

Katika juhudi za kuinua kiwango cha elimu ya msingi kwa wakazi wa Nyamongo, Barrick North Mara kwa kushirkiana na chuo cha ualimu cha Tarime (TTC) na Halmashauri ya wilaya ya Tarime umeanzisha mpango wa kutoa mafunzo ya kuwanoa waalimu wa shule za msingi zipatazo 24 zilizo jirani na mgodi huo.

Hadi mwaka jana tayari wakuu wa shule 24 na waratibu wa elimu wa kata watano wamekwisha nufaika na mafunzo ya uongozi chini ya mpango huo.

Walimu 64 wa madaraja ya B na C wamekwishapata mafunzo ya wiki tatu ya kuinua taaluma yao yaliyofanyika mwanzoni mwa Aprili mwaka huu, katika chuo cha ualimu Tarime.

Mgodi umewajengea Chuo cha Ualimu cha Tarime (TTC) nyumba ya kuishi mwalimu kama motisha ya mwalimu ili aweze kuishi katika mazingira mazuri zaidi.

Mgodi wa North Mara umetumia mamilioni ya pesa kuongezea majengo ya iliyokuwa kituo cha afya cha Sungusungu hadi kuwa hospitali.

Mgodi umejenga wodi nne za kulaza wagonjwa, jengo la upasuaji na kukiwekea kituo hicho cha afya uzio wa waya.

Kuna msemo usemao kuwa penye wengi kuna mengi, idadi kubwa ya watu katika maeneo yenye makazi ya watu na wafanyakazi kutoka mbalimbali lazima yatakuwa na mwingiliano wa kijamii na kimahusiano.

Hivyo mgodi umeanzisha huduma ya kiafya ya AMREF kinachotoa ushauri nasaa na upimaji wa hiari wa virusi vya UKIMWI kilichopo Nyangoto.

Zaidi ya watu 1600 wamekwishapima kwa hiari virusi vya UKIMWI.

Mgodi umejenga shule ya msingi ya Nyabichune ili kuwasaidia wakazi wa Nyamongo kufikia malengo ya kitaifa katika maendeleo ya elimu.

Vilevile vijana yatima tisa wamepata kufundishwa ushonaji na kupewa darasa maalumu katika ofisi ya mgodi idara ya Maendeleo Endelevu na vyerehani vitatu, vitambaa, uzi na vitabu kadhaa.

Katika uhifadhi wa mazingira, ili kupata dhahabu, mgodi umeamua kutumia cyanide badala ya mekyuri. Mekyuri ina madhara kwa afya ya mwanadamu na mazingira kwa ujumla.

Cyanide hayana athari ya muda mrefu kwa mazingira ukilinganisha na mekyuri kwani yenyewe uyeyuka hewani baada ya kupata joto la kawaida sana.

Mwathirika wa Operesheni ilimng’atusha Mwinyi apatikana jalalani


Na Nyasigo Kornel

Mzee Nhalilo Ikerenga Mkigila (65), mmoja wa walioteswa katika ‘operesheni ya wachawi’ mkoani Shinyanga ya mwaka 1974 iliyomfanya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ajiuzulu Uwaziri wa Mambo ya Ndani, anaishi kama mbwa koko jijini Dar es salaam.

Akizungumza na Mtanzania jana Nhalilo ambaye amelemaa mkono na makovu mengi mwilini kutokana na mateso akiwa gerezani, alisema kuwa amekuwa akipata riziki kwa kuokota na kula makombo kwa mama-lishe wa Posta Baharini na kulala stesheni ya reli Posta.

“Watu wengi wanafikiri kuwa mimi ni kichaa, la hasha, mimi nina familia yangu na inaishi Sengerema katika kijiji cha Nyamabano-Nyanzenga, huku nimekuja kutafuta haki zangu na nilipokoswa nauli ya kurudi nyumbani niliona sehemu salama ya kulala ni stesheni kwa maana ni karibu na kituo cha polisi,” alisema Nhalilo.

Alisema kuwa mwaka 1974 Serikali ilieendesha operesheni ya kukamata watu waliotuhumiwa kuwa ni wachawi na ndipo alikumbwa na huo mkasa kijijini kwake Manonga Wilayani Maswa hata kuwekwa mahabusu katika gereza la Nhumbu- Shinyanga sehemu anasema kuwa alikuwa akipata mateso ya kinyama hata kumsababishia athari za kaiafya na hata watu wengine 6 walikamatwa katika mkumbo huo kufa baada ya muda mfupi.

“Tulikuwa tunachapwa kwa viboko, tunapakwa maji ya pilipili kwenye njia ya haja kubwa, kwenye sehemu zilizochubuka baada ya kuchapwa, wanawake walikuwa wakipakwa kwenye sehemu zao za siri, machoni na hata kuna kipindi ilinisababishia upofu,” alisema.

Alisema kuwa wanaume na wanawake katika gereza hilo walikuwa wanavuliwa uchi na kuwekwa sehemu moja huku mateso haya ya kinyama yakiendelea, anasimulia jinsi ambavyo walipokuwa wanaamishwa katika gereza la Mwanholo mkuu wa gereza la kwanza aliwasomea dua akisema.

“Ndugu zangu kutoka Shinyanga naomba Mungu awasaidie mrudi salama, mtakwenda Mwanholo mtakayoyaona huko naomba Mungu awasaidie mrudi salama,” alisema mkuu wa gereza la Nhumbu.

Nhalilo alisema anaidai serikali fidia kwa sababu mahakama ilithibitisha kuwa hawakuwa na hatia na kuachiliwa huru huku yeye akiwa ameathirika kiafya ikiwemo kulemaa mkono na macho yalipopofuka na vilevile alipoteza vifaa vyake vya uganga.

“Mimi nilikuwa ni mganga wa kienyeji na wala sikuwa mchawi, walininyang’anya vifaa vyangu vya uganga na hivyo lazima wanilipe fidia,” alisema.

Ingawaje huyu mzee hana elimu kubwa na kuishi mazingira magumu sana, aliweza kutunza nyaraka zake zote kwenye mkoba wa ngozi aliyokuwa akitembea nayo kila alipokuwa akienda.

Operesheni hii iliendeshwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa (Area Commissioner) kwa kipindi hichi Michael Mabawa ambaye alikuwa akituma polisi kukamata watu waliohisiwa na jamii kuwa ni wachawi.

Michael Mabawa baadaye alistaafishwa kwa manufaa ya umma kama vile Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi alivyostaafu Uwaziri wa Mambo ya Ndani kwa tuhuma ya vitendo hivi vya kinyama kufanyika katika Wizara yake.

Ingawaje hawa walistaafu lakini Mwinyi alikuja baadaye akawa Rais wan chi hii na Michael Mabawa alikuja kugombea tena Ubunge katika jimbo la Magu na kushinda kwa kipindi kimoja kabla ya kuaga dunia.

Nhalilo aliwahi kwenda kupeleka madai yake kwa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) walimpooza tu na kumwambia kuwa arudi kwake Sengerema mpaka watakapomwita, ahadi ambayo haijafanyika mpaka leo.

Kutokana na maelezo yake mzee huyu aliwahi kutoa malalamiko yake mbele ya Hayati Mwl. Julius Nyerere ambapo alipewa nauli za kumrudisha kwake na kisha Mwalimu Nyerere alimwandikia barua ambayo Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Maswa wakati huo akiitwa ‘DD’ alikataa kumpatia, suala linazusha imani yake kuwa Mwalimu Nyerere alimwandikia kujibu madai yake.

Mzee huyu ambaye ndugu zake walikuwa wameshafanya msiba wake mwaka 2005 wakiwa na imani kuwa ameshafariki, habari zake zimepatikana siku chache tu baada ya mtu aliyemtambua kumhoji.

Falsafa ya maandishi ya khanga kwa fikra za mwanamke

Na Nyasigo Kornel

Mwanasaikolojia wa mambo ya ushauri kwa watu walio na fadhaa na mashaka katika maisha (psychotherapist) Dr. John Robert katika kitabu chake kiitwacho ‘The sense of women’, kitabu kilicholaaniwa sana na wanaharakati kuwa kimemwonyesha mwanamke kama kiumbe kinachotumia hisia zaidi kutoa uamuzi kuliko akili.

Dr Robert anasema katika ukurasa wa 12 wa kitabu hicho kuwa mwanamke anaweza akapata tiba ya fadhaa, mashaka, wasiwasi na maudhi yake hata kwa kusoma maandishi chanya (yaani maandishi yanayounga mkono matakwa yake) hata kama inamdanganya na hilo suala haliwezekani.

Hivyo mwanamke aliyekosana na jirani yake mwanamke huweza kujisikia furaha kuvaa khanga yenye maandihi yanayomtetea yeye na kumsimanga jirani yake aliyetofautiana naye hata kama ule ujumbe hauna hauna ukweli.

Mtaalam wa Saikolojia Huston Marawasa aliwahi kuandika katika jarida iitwayo ‘The Riddles’ akiamini kuwa hisia, iwe hasira au furaha zinaweza kurekebishwa na kuwa kwa kiasi cha wastani hata kwa kujilisha kwa taarifa za uongo, ili mradi tu zile taarifa ziwe zimemfikia mhusika kwa namna ya kuiamini.

Na ndio maana katika mashairi ya William Shakespeare aliwahi kuandika huku akijibizana na Othello huku Shakespeare akisema kuwa ‘there is no true love without lies’ (hakuna mapenzi ya kweli bila kuwepo na udanganyifu) na mwishoni mwa shairi hilo anamwambia Othello kuwa ‘when my lover tells me lies, I know that I am cheated but I simply believe’ (ninapoelezwa suala la uongo na mpenzi wangu ninakuwa ninajua kuwa ninadanganywa lakini najikuta naamini).

Haya mawazo ya Shakespeare na Huston yanatoa picha halisi kuwa mtu anaweza akapumbaza fikra zake ili ajijengee imani itakayompa usalama zaidi katika roho kuliko kuwa na mashaka isiyokuwa na majibu yanayoweza kuleta utatuzi wa haraka.

Mzee Felix Hassan Ndonjo ana miaka 67 sasa na aliwahi kuwa mtaalamu wa mavazi, ubunifu na urembo, amewahi kufanya kazi katika kiwanda cha nguo cha Musoma Textile Limited (MUTEX) katika upande wa maandishi ya mavazi.

Ndonjo anasema kuwa yeye alikuwa akiangalia migogoro aliyonayo mwanamke katika msiaha yake ya kila siku na kisha uyatatua kwa njia ya maandishi ya khaga.

“Migogoro ya kifamilia au kati ya familia moja na nyingine ni suala la kawaida lakini utajikuta kwamba wanawake walio wengi ndio waathirika wa majanga ya kijamii, hivyo chuki nyingi za familia huwa katika roho ya mwanamke,” anasema Ndojo.

Ndonjo nasisitiza kuwa maandishi ya khanga ni tiba kwa wanawake wengi na hasa wanawake wa kawaida (anaimanisha mwanamke mwenye elimu ya kiasi na uchumi wa kubangaiza).

Rafiki yake mzee Ndonjo waliyekuwa naye katika idara moja mzee Ogutu Dera mkazi wa Musoma vijijini kwa sasa anasema kuwa yeye alikuwa na uwezo wa kwenda katika mitaa ya uswahilini na kusikiliza masimango ya akina mama na kisha anapata mawazo juu ya falsafa ya kuandika maandishi ya khanga.

Anasema kuwa siku moja alikuwa akilala chumbani kwake katika mtaa wa Iringo karibu kabisa na Bandari ya Musoma, akiwa katika nyumba ile iliyokuwa na wapangaji wengi alisikia mwanamke mmoja akimsengenya mke wake akisema, ‘Maskini akipata matako ulia mbwata’.
“Nilichukua msemo huu wa kawaida na kisha baada ya wiki mbili nilipewa khanga kutoka katika duka la ushirika na niliwauzia kwa mkopo, yule mwanamke alinunua ile ile khanga na kisha kulianika kila siku kwenye kamba mbele ya nyumba yetu ili mradi tu amuumize mke wangu,” anasema mzee Dera.

Khanga ni vazi linalovaliwa na wakazi wengi wa Afrika ya Mashariki ikiwa imeletwa katika karne ya 19 na wafanyabiashara wa Kiindi na Waarabu.

Mwanzoni ilichukuliwa kama bidhaa kwa wakazi wa Pwani tu na hasa hasa Zanzibar, lakini baadaye imekubalika kwa Tanzania yote na sehemu kubwa ya Afrika ya Mashariki na kati.

Khanga inavaliwa sana na wanawake na baadhi ya wanaume ushona mavazi yao kwa kutumia vitenge.

Katika khanga utakuta maandishi yenye misemo, mafumbo na methali mablimbali ambayo mara nyingi umfanya mwanamke kuchagua khanga ya aina Fulani na kuacha nyingine.

Kwa mfano katika khanga utakuta maandishi kama vile ‘Ajabu nazi kavu kutaka kuvunja jiwe’, hapa mwanamke anajivika uhusika wa jiwe na mwenzake anamvika uhusika wa nazi huku yeye akiishawishi fikara zake kuwa anao uimara kama wa jiwe katika hilo suala wanaloling’ang’ania na mwenzake ni dhaifa mbele ya jiwe kama nazi.

Hivyo atakapopita mbele ya mwanamke mwenzake au hasimu wake anajisikia katika roho yake kuwa amekuwa mwamba mbele kwelikweli.

Katika kitabu cha ‘The heart of woman’ mwandishi Handy Casgert anasema kuwa mwanamke ana nguvu nyingi za kijamii moyoni na hivyo masuala ya kijamii na mahusiano yanampa shida nyingi sana kuliko mwanaume na akasema kuwa ujumbe mfupi wa simu za mkononi, ujumbe chanya katika barua, ujumbe chanya wa mziki zina manufaa na tiba kubwa kwa roho ya mwanamke kuliko ya wanaume walio wengi.

Mwisho